1 Oktoba 2019 - 06:41
Marekani yafunga kamandi yake ya Jeshi la Anga Mashariki ya Kati nchini Qatar

Jeshi la Anga la Marekani limetangaza kuhamisha kwa muda kamandi yake ya Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) kutoka Qatar hadi jimbo la Carolina Kusini nchini Marekani.

(ABNA24.com) Jeshi la Anga la Marekani limetangaza kuhamisha kwa muda kamandi yake ya Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) kutoka Qatar hadi jimbo la Carolina Kusini nchini Marekani.

Uamuzi huo wa ghafla umechukuliwa huku Rais Donald Trump wa Marekani akizidisha uhasama wake dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post, Kamandi ya Jeshi la Anga la Marekani katika Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa al-Udeid ilifungwa Jumamosi na sasa oparesheni za kamandi hiyo zitakuwa zikitekelezwa katika Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa Shaw katika jimbo la Carolina Kusini.

Kanali Frederic Coleman, Kamanda wa Kituo cha 609 cha Oparesheni za Anga na Anga za Mbali katika Jeshi la Mareakni amesema Iran imeshatangaza mara kadhaa kupitia njia kadhaa kuwa ina nia ya kushambulia wanajeshi wa Marekani. Aidha amedai kuwa "vita dhidi ya ISIS vinaelekea kumalizika na kuna uwezekano wa muafaka wa amani Afghanistan na kwa msingi huo eneo linaanza kutulia isipokuwa Iran."

Ametoa madai hayo katika hali ambayo utawala wa Trump amekuwa katika mstari wa mbele kuibua taharuki na kuvuruga uthabiti katika eneo la Asia Magharibi kwa kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Aidha utawala wa Trump unavuruga amani na uthabiti kwa kuiwekea Iran vikwazo vilivyo kinyume cha sheria.

Iran imesisitiza mara kadhaa kuwa haitaki vita lakini iko tayari kulinda maslahi yake katika eneo endapo itahujumiwa na Marekani au waitifaki wake.

Pamoja na kuwa Marekani imesema imefunga kituo chake cha kijeshi nchini Qatar lakini bado ina vituo vikubwa vya kijeshi katika nchi kama vile Saudi Arabia, Bahrain, Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu.



/129